Pakua muhtasari huu kama PDF.
Wakati wa dharura ya afya ya umma, watu wanahitaji mawasiliano yaliyo wazi na rahisi kuelewa ili kuchukua hatua na kujilinda. Lakini ukosefu wa kuelewa lugha unaweza kuathiri ufikishaji na ufanisi wa mwitikio. Kama vile mafunzo kutoka kwa mwitikio wa Covid-19 na Ebola yalivyoonyesha, vizuizi vya lugha na mawasiliano:
- Vinapunguza upatikanaji wa habari na huduma kwa makundi ambayo tayari yako katika mazingira magumu.
- Vinaharibu imani ya wanajamii kwa wafanyakazi wa afya na watoa habari za afya.
- Vinapunguza uelewa wa maelekezo kuhusu hatua zinazopendekezwa kama vile chanjo au kwenda kliniki.
- Vinazidisha kuenea kwa uvumi na habari zisizo sahihi.
- Vinazidisha mzigo kwa wafanyakazi wanaokutana na jamii katika mazingira ya lugha nyingi.
Hati hii inatoa mapendekezo ya vitendo kusaidia serikali na watoa msaada kupunguza athari za changamoto zinazohusiana na lugha katika mawasiliano yao na jamii zenye hatari au zinazokabiliwa na mlipuko wa ugonjwa wa Mpox.
Mpox montage based on a photo by Gustavo Fring via Pexels.
Unda data kuhusu matumizi ya lugha katika mipango ya mawasiliano
- Nchi nyingi zilizoathiriwa na mlipuko huu zina utofauti mkubwa wa lugha. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) inaonyesha wingi wa visa vilivyoripotiwa. Lugha za kitaifa na rasmi katika DRC mara nyingi hazieleweki vizuri katika ngazi ya ndani. Watu katika DRC wanaotumia Kiswahili kama lugha ya kwanza au ya pili hutumia Kiswahili cha Kongo; habari katika Kiswahili cha kawaida hazipatikani kirahisi kwa wazungumzaji wa Kiswahili cha Kongo.
- Kujumuisha lugha zote zinazopendekezwa haiwezekani au sio halisi, lakini kutegemea lugha zinazotawala kunawabagua wale walio katika mazingira magumu. Data za matumizi ya lugha zinaweza kusaidia kubaini ni nani atakayefikiwa na ni nani hatafikiwa kupitia mawasiliano katika lugha fulani. Inaweza pia kusaidia kuonyesha ni wapi mawasiliano wazi katika lugha na mifumo ya kimkakati yanaweza kuboresha upatikanaji wa taarifa katika lugha ya pili ya watu.
- Data za matumizi ya lugha zinaweza kusaidia njia iliyo katika muktadha wa mawasiliano. Sifa za milipuko hii zinatofautiana kati ya maeneo na mikoa (aina za virusi). Nchi zingine zinaripoti visa kwa mara ya kwanza, wakati katika nchi nyingine ugonjwa wa Mpox umekuwepo. Mawasiliano yanapaswa kuboreshwa kulingana na uelewa wa mambo watu wanayojua tayari.
Mashirika yanaweza:
- Kufanya uchambuzi wa data za matumizi ya lugha (nani anasema nini, wapi) pale zinapokuwepo. Chunguza ramani za lugha za CLEAR Global na data za matumizi ya lugha kwa baadhi ya nchi zilizoathiriwa na mlipuko huo. Chunguza data mahususi kwa DRC.
- Kukusanya data kuhusu mapendeleo ya lugha ya watu mahali ambapo taarifa za hivi karibuni zinakosekana au watu walioathiriwa wana uwezekano mkubwa kuwa na utofauti wa lugha (kwa mfano, jamii za mipakani, watu waliotawanywa, utofauti mkubwa wa kikabila, kabila au ukoo). Angalau, uliza “Lugha kuu unayotumia nyumbani ni ipi?”
- Kulinganisha data za matumizi ya lugha na data za maeneo ya mlipuko ili kusaidia kutathmini ufikaji wa mawasiliano.
- Kushiriki data kuhusu matumizi ya lugha na uchambuzi unaohusiana kati ya mashirika yanayoshughulikia.
- Kumbuka kuwa si sahihi au halisi kudhani kwamba wafanyakazi wa ndani au wanajamii wanaelewa kiwango chote cha mapendeleo ya lugha ya jamii.
Weka kipaumbele kwenye mawasiliano wazi kwa lugha rahisi
- Kuandika taarifa kwa lugha rahisi kunaweza kuboresha sana uelewa, hasa kwa watu ambao hawazungumzi lugha hiyo kwa ufasaha au ambao sio wataalamu wa afya. Pia kunaboresha usahihi wa tafsiri, hasa wakati watu wanapofanya tafsiri au kukalimani papo hapo.
- Maneno yanayofikiriwa kuwa rahisi kueleweka yanaweza bado kusababisha mkanganyiko kwa lugha au makundi fulani. Jaribio la matumizi ya istilahi za Ebola kwa Kifaransa na Kiswahili cha kawaida nchini DRC liligundua kwamba hata maneno rahisi kama chanjo, fomu, idhini, na damu yalikuwa hayaeleweki. Jaribio la vifaa vya kuhamasisha chanjo kwa wazungumzaji wa lahaja tofauti za Kisomali liligundua kwamba maneno kama virusi, homa, chanjo, dalili, na kujitenga huenda hayakueleweka vizuri.
- Zaidi ya changamoto za uelewa, maneno yasiyo wazi yanaweza kuongeza sana kukosa uaminifu na hofu kwa wafanyakazi wa afya. Hii inachochea habari za uwongo zenye madhara na kuathiri sana watu wanapotaka kutafuta huduma.
- Uelewa wa lugha unachangia jukumu muhimu la watoa mawasiliano wa ndani. Watangazaji wa redio, shule, vikundi vya kidini, na wadau wengine wa jamii mara nyingi hufanya ‘tafiti papo hapo’ (kutafsiri mara moja) taarifa rasmi katika lugha za jamii. Lakini wanaweza kuwa na ugumu kuelewa na kuwasilisha kwa usahihi, na kuongeza hatari ya habari potofu kwa wanajamii.
- Uelewa wa lugha unaweza kuboresha sana uelewa na utekelezaji wa hatua kama vile chanjo. Watu wana uwezekano mkubwa wa kuamini chanjo wanapopata taarifa na wanaweza kuuliza maswali kwa lugha wanayoihisi kuwa rahisi kutumia. Kwa ujumla, uaminifu uko juu zaidi kati ya watu wanaoshiriki lugha ya kwanza.
- Mawasiliano ya kuona yanaweza kuwa na faida katika kuwasiliana kuepuka vizuizi vya lugha, lakini hayakueleweka kote kote. Rangi, mpangilio, alama, nguo na nyuso, asili na vipengele vingine vya kuona vinatafsiriwa tofauti katika makundi na lugha tofauti na hili linaweza kusababisha kuchanganyikiwa na kutokuelewana.
- Mawasiliano mabaya yanaweza kuongeza aibu iliyopo kuhusu mpox. Hii inahatari ya kuendeleza habari potofu, kama vile dhana kwamba mpox unaenezwa tu kupitia vitendo vya ngono.
Mashirika yanaweza:
- Kuandika taarifa kwa ajili ya jamii na watoa mawasiliano wa ndani kwa lugha rahisi.
- Kujaribu vifaa vya mawasiliano kuhusu hatari inapowezekana na kupima maneno yote yanayotumika. Hata kama tafsiri kamili haijapangwa, jumuisha jamii tofauti za lugha katika majaribio ili kubaini ni kwa kiwango gani vifaa vinaweza kueleweka katika lugha za pili au tatu, au wakati watu wanaweza kuelewa tu misemo rahisi. Kutumia maarifa hayo kubaini mapungufu muhimu katika utoaji wa taarifa.
- Kuwaapa watoa mawasiliano na wafanyakazi wa afya katika mazingira ya lugha nyingi (kwa mfano, kambi za wakimbizi) msaada halisi wa lugha wa kama vile kamusi za maneno muhimu au vifaa vya kuona.
- Wakati wasomi wa lugha hawapatikani, kuwapa watu wenye ujuzi wa lugha husika mafunzo ya msingi ya tafsiri ili kurahisisha mawasiliano ya lugha nyingi.
Shughulikia masuala ya lugha na mawasiliano kwa makundi maalum
- Kiwango cha maambukizi na uenezi miongoni mwa watoto kiko juu zaidi kuliko milipuko ya zamani ya mpox, hivyo mawasiliano yanayofaa kwa watoto ni muhimu sana. Baadhi ya vifaa vinavyowasiliana na watoto vimeandaliwa lakini huenda havipo katika lugha zinazohusika. Wazazi na walezi wanahitaji taarifa wazi na rahisi kufikiwa ili waweze kuwasiliana na watoto kuhusu kuzuia uenezi na kutambua dalili.
- Wafanyabiashara ya ngono wanahitaji taarifa wazi ili kusaidia kuelewa jinsi ya kujilinda. Aibu na ubaguzi wa awali vinaongeza changamoto za lugha na mawasiliano kwa wafanyakazi wa ngono, ambao wanaweza kutokuwa na uaminifu au kuwa na ufikiaji mdogo wa taarifa rasmi.
- Jamii za mipakani, wahamiaji wa ndani, na wakimbizi zina utofauti wa lugha. Watu wanaweza kupendelea taarifa za maandisho katika lugha moja na taarifa za kuzungumzwa katika lugha nyingine, kulingana na jinsi walivyopata elimu au kujifunza lugha za jamii mwenyeji. Watoa mawasiliano wa afya huenda wasiweze kuzungumza (lugha zote) zinazohusika kwa hadhira yao katika muktadha huu.
Mashirika yanaweza:
- Kuweka kipaumbele kwenye mawasiliano ya sauti na ya ana kwa ana, hasa ili kuwafikia wanawake na makundi yasiyojua kusoma na kuandikaau ufikiaji duni wa elimu.
- Pale ambapo kuna bajeti ya msaada wa lugha (kwa mfano, kutafsiri), kuzingatia kutengwa kwa lugha katika kupanga pamoja na hatari zingine ili kusaidia kugawa rasilimali kwa wale walio katika hatari zaidi.
- Kufanya majaribio ya vifaa na makundi tofauti ya watoto kwa umri, na wazazi au walezi wao. Jumuisha wazungumzaji wa lugha tofauti ili kubaini ni nani atakayeelewa au kukubali vifaa na ni nani asiyekubali.
- Kushirikiana na mashirika ya watu wenye ulemavu kuhusu mifumo ya mawasiliano inayoweza kuwafikia.
- Kuwa na ufahamu kuhusu jukumu la lugha katika kuimarisha uaminifu na kupambana na aibu unaponawasiliana na wafanyakazi wa ngono na makundi mengine katika hatari ya ubaguzi na kutengwa.
- Kufuatilia upatikanaji na matumizi ya hatua za afya ya umma kwa kutumia lugha na takwimu nyingine za demografia (jinsia, umri, ulemavu, kiwango cha elimu) ili kubaini maeneo ambapo lugha inaweza kuongeza kutengwa kwa makundi fulani.
Jinsi CLEAR Global inavyoweza kusaidia
Dhamira ya CLEAR Global ni kuwasaidia watu kupata taarifa muhimu na kusikilizwa, bila kujali lugha wanayozungumza. Tunawasaidia mashirika washirika wetu kusikiliza na kuwasiliana kwa ufanisi na jamii wanazohudumia. Tunatafsiri ujumbe na nyaraka katika lugha za kienyeji, kusaidia tafsiri za sauti na taarifa za picha, kuwafundisha wafanyakazi na wajitoleaji, na kutoa ushauri kuhusu mawasiliano ya pande mbili. Pia tunashirikiana na washirika kufanya majaribio ya vifaa na kuyarekebisha ili kuboresha uelewa na athari, na kuunda suluhisho za teknolojia ya lugha zinazofaa kwa jamii. Kazi hii inaongozwa na utafiti, ramani za lugha, na tathmini za mahitaji ya mawasiliano ya jamii lengwa.
Pia tunatoa mafunzo kusaidia mawasiliano ya kibinadamu yenye ufanisi (masuala yanajumuisha tafsiri ya kibinadamu, mawasiliano katika dharura, na lugha nyepesi). Kwa maelezo zaidi, tembelea tovuti yetu au wasiliana nasi kupitia info@clearglobal.org.